Showing posts with label jamii. Show all posts
Showing posts with label jamii. Show all posts

Tuesday, September 18, 2012

MKUU WA MKOA ATATUA MGOGORO WA SHULE KATI YA WANANCHI




 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Massawe Akiwahutubia Wananchi wa Kata ya Katoke Kabla ya Kuwakabidhi Shule yao Eneo la Kimbugu.
 Jengo la Utawala la Shule ya Sekondari ya Wasichana Ambayo Ruth Blasio Msafiri Anadai ni Mali yake, Tayari Imekadhiwa kwa Wananchi
 Wananchi wa Kata ya Katoke Wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Muleba na Diwani wa Kata Hiyo Kwenda Kwenye Eneo la Shule Kukabidhiwa Majengo ya Shule hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe hatimaye ametatua mgogoro wa shule ya sekondari ya Wasichana ya Ruth Msafiri kati ya Wananchi na aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Muleba Kaskazini Ruth Blasio Msafiri kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi 2010.
 
Mhe. Massawe alikabidhi shule hiyo kwa Wananchi wa Kata ya Katoke jana tarehe 17/09/2012 ili waendeleze ujenzi baada ya kuwa na mgogoro zaidi ya miaka miwili kati ya Wananchi na aliyekuwa mbunge wao 2005 hadi 2010 kwa kudai shule hiyo ni mali yake binafsi baada ya kuwa ameshindwa ubunge mwaka 2010. 
 
Shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana ya Ruth Msafiri iliyoko katika kitongoji cha Kimbugu, Kijiji Katoke Tarafa Izigo Halmashauri ya Wilaya Muleba ilianzishwa na Ruth Blasio Msafiri wakati huo akiwa Mbuge wa Jimbo la Muleba Kaskazini mwaka  2009.
 
Kulingana na taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi na seriklai ya kijiji Katoke Ruth Msafiri alitoa wazo la kuanzisha shule ya wasichana na kuomba ardhi katika serikali ya kijiji na kupewa Ekari 40 za ardhi kwa kuwa walikubaliana shule hiyo iwe ya wananchi wa Kata ya Katoke.
 
Pia wananchi walikubaliana shule hiyo iitwe kwa jina la Ruth Msafiri baada ya kuwa yeye ndiye aliyeanzisha wazo la kuwa na shule ya wasichana katika kata hiyo. Vilevile Bi Ruth Msafiri alianza kuomba michango kwa niaba ya wananchi  ili kuanzisha ujenzi wa shule hiyo mwaka 2009. 
 
Wananchi walichangia nguvu zao pia mfuko wa jimbo ulichangia Shilingi 3,000,000/=, Benki ya NMB ilichangia shilingi 5,000,000/= Wizara ya Maliasili na Utalii shilingi 6,000,000/=, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kikwete alichangia mabati 300 na ndipo ujenzi wa shule hiyo ulianza.
 
Baada ya uchaguzi Mkuu 2010 Ruth Msafiri hakubahatika kuchaguliwa tena kuliwakilisha jimbo la Muleba Kaskazini na ndipo mgogoro ulianza na akadai kuwa shule ni mali yake jambo ambalo wananchi hawakukubaliana naye na kuanza kulalamika na malalamiko hayo yalimfikia Mkuu wa Mkoa.
 
Tarehe 20/02/2012 Mkuu wa Mkoa alitembelea kijiji cha Katoke na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi na alisikiliza mgogoro huo kwa undani na akaagiza wananchi wapitie kwenye ngazi husika za kisheria kuanzia ngazi ya kijiji Balaza la Kata na Balaza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ili kulidhia kuwa shule hiyo ni mali ya wananchi.
 
Aidha baada ya hatua zote Mkuu wa Mkoa alizoagiza  kufuatwa nay eye kuridhia jana tarehe 17/9/2012 Mhe. Massawe aliikabidhi shule hiyo kwa wananchi ili kuendeleza ujenzi kwaajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2013. 
 
Kutokana na furaha ya kukabidhiwa shule yao wananchi wakiongozwa na Mhe. Massawe na Mkuu wa Wilaya ya Muleba walianza kuchangia ujenzi wa shule hiyo kwa kutoa fedha taslim, ahadi na zaidi ya shilingi 1,800,000/= zilichangwa pia mawe, mchanga, sementi, misumari na mbao vilihaidiwa kuchangiwa na wananchi hao.  
 
Shule hiyo ina jengo la utawala pia na vyumba viwili vilivyo pauliwa tayari, na msingi wa vyumba vitatu ambavyo havijakamilika. Wananchi walimhaidi Mkuu wa Mkoa kufikia mwezi Oktoba 2012 majengo hayo tayari yatakuwa yamekamilika kwa ajili ya Januari mwakani.
 
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Aliyeruka Juu Akicheza Ngoma ya Kihaya Baada ya Kuwakabidhi Wananchi Shule yao Aliungana nao  Baada ya Kuona Walivyofurahi Sana Kukabidhiwa Shule na Kuwa ya Jamii

Imetolewa na:
Sylvester Raphael
Afisa Habari Mkoa,
Kagera @2012

Dk Magufuli aombwa kumulika malipo ya fidia Kyaka-Bugene




Mzee Theobard Kishenye akiondoka katika hali ya kukata tamaa katika ofisi za Wilaya ya Karagwe baada ya jina lake kukosekana kwa wanaotakiwa kupewa fidia
Mbunge wa viti maalumu CCM Bernadetha Mushashu akisikiliza malalamiko ya baadhi ya wananchi wa wilaya ya Karagwe ambao hawatapata fidia kupisha ujenzi wa barabara ya Kyaka-Bugene
BAADHI ya wakazi wa Wilaya ya Karagwe wamemuomba Waziri wa Ujenzi Pombe Magufuli kumulika zoezi la ulipaji wa fidia ya kupisha ujenzi wa barabara ya Kyaka Bugene kwa madai kuwa uthamini  wa mali ulifanyika kwa upendeleo.
Wananchi wa vijiji vya Kihanga na Kishao wametoa kilio hicho baada ya kubainika kuwa katika orodha ya watakaolipwa fidia  zipo nyumba zilizojengwa miaka ya karibuni huku zenye miaka zaidi ya hamsini zikiondolewa katika orodha ya kufidiwa.
 Mkazi wa kijiji cha Kishao Magreth Peter ambaye ni mama mjane alisema amejulishwa na Tanroads Mkoa wa Kagera kuwa nyumba yake itabomolewa bila fidia,wakati huo jirani zake ambao wako ndani ya mita 22.5 kama yeye wakiwa wameanza kulipwa.
Mwananchi mwingine wa kijiji hicho Adventina Furuka ambaye pia ni mjane alishangazwa na baadhi ya nyumba za kifahari zilizojengwa miaka ya karibuni katika ukanda ule ule  kuonekana katika orodha ya watakaolipwa huku wao majina yakikosekana.
“Nimeolewa hapa tangu mwaka 1950 naishi na watoto na wajukuu ,nimeambiwa nyumba yangu itabomolewa bila kulipwa fidia wazee wote wamezikwa hapa nyumbani na kuna makaburi saba”anabainisha mama huyo.
Pia waliwatuhumu walioendesha zoezi la utahamini baada ya kudaiwa kuwataka wale wenye nyumba zenye umri mkubwa kupeleka uthibitisho wa stakabadhi za kununua  mabati ya kuezekea ili waingizwe kwenye orodha ya watakaofidiwa.
Aidha mzee Theobard Kishenye alidai zoezi la uthamini lilijaa mazingira yenye utata kwani baadhi ya wananchi waliitwa kwa ajili ya majadiliano na walioendesha zoezi hilo.Alisema majirani zake walioko kwenye mita zile zile wameanza kupokea malipo na kuwa amejulishwa kuwa hatalipwa fidia.
Naye Mchungaji Japhet Runyoro alisema kuna utata mkubwa katika majina yaliyopitishwa kwa ajili ya fidia ikiwemo nyumba mpya za hivi karibuni na kutaka Waziri Magufuli kuingilia kati suala la malipo ya wananchi wanaotakiwa kupisha ujenzi wa barabara.
Naye ofisa wa Tanroads Mkoa wa Kagera Gasper Kyaruzi aliyekuwa akitoa malipo ya fidia juzi kwa baadhi ya wananchi  alikataa kutoa ufafanuzi kwa kundi kubwa la wananchi waliokuwa wakidai hawana imani na zoezi la uthamni lilivyoendeshwa.
Alisema kazi aliyokuwa ametumwa ni kulipa fedha kwa  wananchi wanaostahili fidia ambao pia majina yao yalikuwa yametundikwa katika mbao za matangazo katika Halmashauri ya Wilaya hiyo na kuwa mwenye malalamiko ayapeleke ofisi za Tanroad Mkoa.

Picha Mbalimbali za Wiki Ya Nenda Kwa Usalama Barabarani Bukoba




Wasanii wa kikundi cha sanaa cha KAKAU wakitumbuiza wakati wa ufunguzi wa sherehe za maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama yaliyofunguliwa na mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe kwenye uwanja wa michezo wa Kaitaba.




Baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Kagera wakiwa ndani ya uwanja wa kaitaba wakisubili ufunguzi wa sherehe za maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama.




Massawe akionyeshwa kifaa kinachokagua ubora wa mataili.




Massawe akiwa amesimama wakati akipokea maandamano.




Massawe, akipewa maelezo na PC Fadhil juu ya kifaa kinachodhibiti mwendo kasi.




Mkuu wa mkoa wa Kagera akisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na PC Alexander juu ya alama za barabara.




PC Alexander ambaye ni mkaguzi wa magari wa kitengo cha usalama barabarani mkoani Kagera akimuelezea Massawe mambo yanayohusiana na alama za barabara.




Baadhi ya magari yakiingia kwenye uwanja wa michezo wa kaitaba wakati wa uzinduzi wa sherehe za maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama.




Waendesha pikipiki wakiandamana wakati wa uzinduzi wa wiki ya usalama barabarani.

Maisha Yanaendelea


Wassira Mgeni Rasmi Gwaride Herritage Schools











Katika pitapita kamera ya mjengwablog iliweza kunasa tukio hili kutokea mbali maeneo ya water front Dar,ambapo Mh Steven Wassira alionekana akikagua gwaride la kilichoitwa wanafunzi wa shule  za herritage
Hatukuweza kujua hasa ilikuwa ni shughuli inayohusu nini.
Mdau wa mjengwablog,Dar.

Magazeti Magazeti









Ugumba Wawatesa Watanzania Wengi



Na: Florence Majani na Herieth Makwetta. Mwananchi
TATIZO la uzazi linaonekana kushika kasi nchini baada ya idadi kubwa ya wanandoa kukimbilia Kenya kupata huduma ya upandikizaji wa watoto kwa gharama ya zaidi ya Sh5 milioni.Kati ya wageni 10 wanaokwenda katika vituo vya upandikizaji vya Aga Khan na Nairobi IVF Centre nchini humo, wanne wanatoka Tanzania.

Licha ya kuwapo kwa huduma hiyo nchini, imeelezwa kwamba Watanzania wengi wanakimbilia huko kutokana na unafuu wa gharama na ubora wa huduma.

Huduma hiyo ni ya mwanamke kupandikizwa mbegu ya kiume ili kuweza kushika mimba na baadaye kupata mtoto.
Mmiliki wa Kituo cha Upandikizaji cha Nairobi (Nairobi IVF Centre), Dk Joshua Noreh alisema kwa mwaka kliniki yake hupokea zaidi ya wagonjwa 270 kutoka mataifa mbalimbali likiwamo Bara la Ulaya.

Alisema wagonjwa kutoka Tanzania walianza kumiminika katika kliniki hiyo kuanzia mwaka 2006 na ukiondoa gharama za matibabu ambazo ni Sh5.4 milioni zipo gharama za ushauri na uchunguzi wa tatizo.

“Gharama ya ushauri peke yake ni Sh42,000 za Tanzania. Baada ya ushauri, mgonjwa hutozwa Sh420,000 kwa ajili ya uchunguzi wa tatizo. Gharama za matibabu hutegemea ukubwa wa tatizo. Tiba yenyewe ni upandikizaji wa mbegu, hadi hatua za kuirutubisha,” alisema.

Dk Noreh alisema ukijumlisha gharama za usafiri, malazi, mlo na tiba kwa wagonjwa wanaotoka Tanzania, wengi wao hutumia kati ya Sh8milioni hadi Sh10 milioni, kwa ajili ya kupata mimba.

Imeelezwa kuwa raia wa Uganda hukimbilia Kenya kukwepa gharama kubwa kwani nchini humo hugharimu kiasi cha Sh500,000 ya Uganda (sawa na Sh9.5 milioni) wakati huduma hiyo hupatikana Kenya kwa Sh300,000 (sawa na Sh5.4 milioni) kwa mzunguko.

“Tuna vituo zaidi ya vitano vya IVF hapa Kenya, ndiyo maana Kenya imekuwa kimbilio la wanandoa au wapenzi kupata matibabu ya aina mbalimbali za ugumba. Lakini kikubwa ni huduma bora na gharama nafuu ndiyo sababu ya ongezeko hili la wageni kutoka nje.”

Alisema baadhi ya nchi hazina huduma ya IVF hivyo wanandoa huenda Kenya na wengine wanayo huduma hiyo katika nchi zao ila wanachagua Kenya kwa sababu ya urahisi wa tiba hiyo na kuwapo kwa mbegu za wanaume wa Kiafrika zilizohifadhiwa.

Nchi nyingine ambazo wanandoa wake wanaongoza kwenda Kenya kwa ajili ya kupata huduma ya upandikizaji wa watoto ni Uganda, Sudan ya Kusini, Marekani na Ethiopia.

Mtaalamu kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan Nairobi, Dk Prafull Patel alisema idadi ya wanaohitaji huduma hiyo imekuwa ikiongezeka kwa kasi kutoka mataifa ya Afrika, Uingereza na Marekani.

Alisema zaidi ya robo tatu ya wanaopata huduma hiyo ni watu kutoka nje ya Kenya, lakini hasa ni kutokana na unafuu wa gharama za huduma hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine.

Nchini Uganda, IVF inagharimu Sh9,000,000 za Tanzania wakati Uingereza inagharimu zaidi ya Sh10,800,000 za Tanzania na kwa wenza zinafikia Sh21,600,000 kwa kila mzunguko huku Marekani ikigharimu Sh10,620,000 na Sh19,800,000 kwa mzunguko.

Hii inamaanisha kwamba gharama nchini Kenya ni nusu ya gharama inayolipiwa Marekani, Ulaya na nchi nyingine za Afrika. Hiyo inaelezwa kuwa chanzo cha ongezeko la idadi ya wageni kwenda Kenya kusaka tiba ya ugumba.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz

Wahariri Saccos Development Yaanzishwa Jijini Dar es salaam



 Mwenyekiti wa wamiliki vyombo vya habari nchini (MOAT) Ndugu Reginald Mengi akimkabidhi Daniel Chongolo hati za usajili wa WAHARIRI DEVELOPMENT SACCOS kwenye hafla fupi iliyafanyika Karimjee Hall,Dar es salaam


Wadau mbalimbali waliojitokeza kwenye uzinduzi wa WAHARIRI DEVELOPMENT SACCOS kwenye hafla fupi iliyafanyika pale Karimjee Hall,Dar es salaam

Reactions::

JK Aweka Jiwe La Msingi Kuzindua Rasmi Ujenzi Wa Barabara Ya Bagamoyo-Msata


Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiweka jiwe la msingi kuzindua rasmi ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo-Msata uliofanyika katika kijiji cha Kiwangwa wilayani Bagamoyo leo mchana.Wengine katika picha kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi, Kaimu Mkuu wa mkoa wa Pwani ambaye pia ni mkuu  wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik(Wapili kushoto),Waziri wa Ujenzi Dkt.John Pombe Magufuli(wanne kushoto) na kulia ni Waziri wa Mazingira Mhe. Theresa Hoviza.

Ndoto ya miaka mingi ya kujengwa kwa barabara ya Msata-Bagamoyo kwa kiwango cha lami imetimia leo, Jumanne, Septemba 18, 2012, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipoweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara hiyo katika sherehe kubwa iliyofanyika eneo la Kiwangwa.
Barabara hiyo ya kilomita 64 inajengwa na mkandarasi wa ndani ya nchi, Estim Construction, na inagharimiwa asilimia mia na Serikali ya Tanzania bila msaada kutoka kwa mfadhili yoyote.Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania, Injinia Patrick L. Mfugale amesema kuwa barabara hiyo inayogharimu kiasi cha Sh. bilioni 94, ikiwa ni pamoja na fedha za fidia na kumlipa mkandarasi mshauri, itakamilika Juni mwakani.

Pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais ameweka jiwe la msingi kwenye barabara hiyo, Injinia Mfugale amesema kuwa mkandarasi wa sasa alianza ujenzi tokea 2010 baada ya usanifu wa barabara hiyo kukamilika na baada ya Serikali kumtimua mkandarasi wa mwanzo wa barabara hiyo, TACOPA, Novemba 13, mwaka 2009.Amesema kuwa mpaka sasa barabara hiyo imekamilika kwa asilimia 65, yaani kwamba kiasi cha kilomita 36.7 tayari zimewekwa lami na kuwa ni kilomita 23 zilizosalia na ambazo zitamalizika katika miezi tisa ijayo.Injinia Mfugale amesema kuwa mpaka sasa Serikali imekwishakulipa kiasi cha Sh. bilioni 56.8 ikiwa ni pamoja na fedha iliyolipwa kama fidia kwa wananchi ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo.Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo hautahusisha ujenzi wa daraja kwenye Mto Ruvu kwa sababu usanifu wa daraja hilo ulichelewa kidogo kukamilika hata kama tayari sasa umekamilishwa.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John P. Magufuli amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya ujenzi wa kilomita 11,154 za barabara za lami zinazojengwa na Serikali ya Mheshimiwa Kikwete.“Nataka muelewe vizuri maana ya kilomita hizi. Wakati wa Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, tulikuwa na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 1,330. Kati ya Uhuru na mwaka 2005, tulijenga barabara zenye urefu wa kilomita 6,500 na kati ya 2005 na sasa tunajenga barabara zenye urefu wa kilomita 11,154,” amesema Waziri Magufuli.Waziri huyo amerudia msimamo wake kuwa kamwe Serikali haitawaachia watu wanaojenga ama kufanya shughuli katika eneo la hifadhi ya barabara bila kuwachukulia hatua.

Naye Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi walioshiriki katika sherehe hizo kuwa barabara ndiyo mishipa ya damu ya uchumi wa nchi yoyote na ndiyo maana Serikali inatenga kiasi kikubwa katika Bajeti yake kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Amesema kuwa katika Bajeti ya sasa, barabara zimetengewa kiasi cha Sh. trilioni 2.2 ambacho ni kiasi kikubwa cha pili baada ya Bajeti ya elimu.Rais Kikwete amesema kuwa pamoja na faida zake kubwa na nyingi, barabara hiyo itakuwa na changamoto zake ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ajali za barabara, kuongeza urahisi wa kusambaa kwa ugonjwa wa ukimwi na hata kuvutia watu wenye lengo la kununua ardhi kubwa ya wanavijiji ambako inapita barabara hiyo.Rais pia ameungana na Waziri Magufuli kwa kuonya: “Kama alivyosema Waziri, wanaoifuata barabara watavunjiwa nyumba zao na hawatalipwa, lakini wale ambao barabara inawafuata watalipwa hata wakivunjiwa.”

Imetolewa na:Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu.Dar es Salaam. 18 Septemba, 2012

Thursday, September 13, 2012

Picha Mbali Mbali




Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali mstaafu Fabian Massawe akishiriki kwenye zoezi la usafi katika manispaa ya Bukoba.




Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba Khamis Kaputah akimueleza Kanali Massawe mikakati ya kuliondoa dampo la Kashai.




Massawe akiangalia dampo la lililoko eneo la Kashai.



Dampo lililoko kwenye maeneo ya soko la Kashai.




Vijana wakimshangilia Massawe 




7146 Waziri Mkuu, Mizengo Pindanda na Mkewe Tunu (kushoto) wakivuka katika Pantoni ya MV Ujenzi kutoka Kisorya hadi Rugezi Ukerewe wakiwa katika ziara ya mkoa wa Mwanza Septemba 11, 2012. Aliyekaa kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarest Ndikilo na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



Abiria wakisafiri na mizigo yao kati ya Rugezi wilayani Ukerewe na Kisorya wilayani Bunda, Septemba 11, 2012. Ingawa serikali imenunua kivuko kipya chenye uwezo wa kubeba abiria, mizigo na magari bado badhi ya watu wanalipa nauli na kusafiri kwa mitumbwi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)




Basi lenye namba za usajili T329 AMD likiwa limesheni mizigo kuliko uwezo wake likielekea Itigi. Basi hilo lilikuwa likisafiri katika barabara ya Tabora-Itigi-Manyoni mwishoni mwa wiki iliyopita kama lilivyokutwa karibu na stesheni ya reli ya Kazi-Kazi. (Picha na Irene Bwire)



Wamachinga wakiuza bidhaa mbalimbali kwenye mtaa ulioko kwenye barabara ya kuelekea hospitali ya kuu mkoa wa Kagera, halmashauri ya manispaa ya Bukoba ilishawahi kuwapiga marufuku wanachinga kuuza bidhaa zao kwenye eneo hilo, pamoja na amri hiyo wamachinga wameanza kurejea kimyakimya kwenye eneo hilo na kuendelea na biashara yao.




Wanachinga wakiuza bidhaa zao kwenye maeneo yalizuiliwa.




Usafi unaoonekana kwenye barabara za halmashauri ya manispaa ya Bukoba zinatokana na jitihada za Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe, inayoonekana ni barabara ya Kashozi.




Mtaa wa Hoteli ya Lwabizi Plaz



Mamdhari ya mitaa ya halmashauri ya manispaa ya Bukoba.




Barabara ya kuelekea mtaa wa Kashenyi uliko katika kata Kashai ambayo ilikuwa inapitika kwa shida sasa manispaa ya halmashauri ya Bukoba imeanza kuifanyia ukarabati wa kina.




Sehemu ya barabara ya Kashenye